Thursday 5 January 2017

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humprey Polepole atangaza neema kwa Wanafunzi waliokosa mikopo

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM, Humprey Polepole amewatangazia neema wanafunzi wa elimu ya juu waliokosa mikopo, akiwataka wamtafute ili awaoneshe cha kufanya

Polepole ambaye alikuwa kwenye kipindi cha Kikaangoni cha EATV aliuzwa na baadhi ya watu kuhusu tatizo lililopo la mikopo ya elimu ya juu, ambapo aliwajibu kuwa serikali imekwishatoa maelekezo kwamba haiwezi kumkopesha kila mtu na kwamba inatoa mikopo kwa vigezo vilivyowekwa.

Kuhusu watu wasioweza kujigharamia elimu hiyo na wamekosa mikopo, amewashauri kuahirisha masomo yao, ili wafanye kazi ambazo zitawasaidia kupata pesa na ndani ya mwaka mmoja ana uhakika watakuwa wamepata pesa zinazohitajika na kuendelea na masomo yao.

Polepole alitaja baadhi ya shughuli ambazo angewashauri wazifanye kuwa ni pamoja na kilimo huku akitolea mfano baadhi ya watu aliowashauri wajiingize kwenye kilimo cha matikiti na wakaufanyia kazi ushauri huo, ambapo baada ya muda wameona matunda yake.

"Waliokosa mikopo vyuo vikuu wanitafute, nitawaonesha cha kufanya, na wawe tayari kuahirisha masomo mwaka mmoja"

Akizungumzia uamuzi wa serikali kusimamisha ajira, Polepole amesema serikali haiwezi kuendelea kuajiri wakati inafanya kazi ya kuondoa wafanyakazi hewa ambao wanalitia hasara taifa na kuwataka watanzania waendelee kuwa watulivu na kumuunga mkono Rais Magufuli, ili amalize mchwa wote serikali na kisha ajira zitatoka.

"Nawaambia vijana wakati unasubiri ajira usibweteke kwani mtu anayebweteka akipata kazi ataharibu kazi yetu"

Kuhusu serikali kuajiri walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati pekee, Polepole amesema uamuzi huo ni sahihi kwa kuwa taifa lina uhaba mkubwa wa walimu wa Sayansi na Hisabati kuliko walimu wa masomo ya sanaa.

"Tunao utimilifu wa walimu wa sanaa, tunao upungufu wa walimu wa Sayansi"
habari mpekuzihuru

Kafulila kupokea kadi ya Chadema jimboni Kwake Mwezi Huu

Aliyekuwa  Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amesema atapokelea kadi ya Chadema jimboni mwake baadaye mwezi huu.

Kafulila alitangaza kuhama NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema kwa alichoeleza kuwa ndicho chama kilichojipambanua kuelekea safari ya mabadiliko ifikapo mwaka 2020.

Kada huyo tayari amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kuwa anajivua uanachama na  anarudi Chadema.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Kafulila alisema ameamua kuwa atapokelea kadi hiyo jimboni kutokana na mapenzi aliyonayo kwa wananchi wake.

"Nimepanga kuchukua kadi mwezi huu jimboni, kwa kuwa ilikuwa nichukue kadi mwanzoni lakini ilishindikana kutokana na siku kuu, hivyo siku yoyote kuanzia sasa nitachukua," alisema.

Wakati anajiuzulu NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema, alisema hakufanya uamuzi kwa kukurupuka bali alitafakari na kushauriwa na wananchi wa jimbo lake, na kuridhika kurudi huko.

"Nilitafakari na kushauriwa sana jimboni na kuridhika kwamba Chadema ndiko sehemu inayojipambanua kwa mikakati ya kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania na ni vema kukusanya nguvu ya kila mwenye kiu ya mabadiliko ndani ya chama kimoja, ili kufupisha safari ya mabadiliko," alisema.

Alipoulizwa kwa nini amerudi Chadema wakati aliyekuwa Katibu  Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa alipata kumwita sisimizi kwa  alichoeleza kuwa hakuwa na imani naye, alijibu kuwa siasa ni malengo si uhusiano binafsi.

Kafulila aliongeza kuwa wanasiasa wanaunganishwa na malengo zaidi ya urafiki na kwamba malengo yake sasa ni kuendelea kupigania mabadiliko ya kimfumo yanayoenea zaidi kwenye chama hicho (Chadema) kuliko kingine.

Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua uanachama wa Chadema na kuhamia NCCR-Mageuzi kutokana na kuondolewa kwenye nafasi ya uofisa habari wa chama hicho.

Pia akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa uanachama kwa kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka 'kumpindua' Mwenyekiti, James Mbatia.

Hata hivyo, suala hilo lilipata suluhu baada ya Mbatia kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Mbunge. Wakiwa bungeni, Mbatia na Kafulila walikutana, kuzungumza na hatimaye kumaliza mzozo wao.
habari mpekuzihuru

Waziri Mkuu aagiza akiba ya mahindi itunzwe hadi msimu ujao wa Mavuno........ RC, Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.

“Angalieni ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”

“Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,”alisisitiza.

“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,”alisisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.

Alisema kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.

“Kanda ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.

“Kanda ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu utakapokamilika.”

Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.

Alipolizwa ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila mwaka).

“Kuimarika kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. 

“Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.

Waziri Mkuu leo anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
habari mpekuzihuru

Waziri Mkuu apiga marufuku Madiwani kupewa fedha za maendeleo mikononi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini kuacha kutoa fedha taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.

Badala yake amewataka waandae mfumo maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za mfuko wa Jimbo ambazo ni maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za maendeleo jimboni.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo Manispaa ya Songea.

“Nimepata taarifa kuwa fedha za maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana. Msiwape fedha mkononi, bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na matumizi ya aina hiyo, mwisho wake ni jana,” alisisitiza.

“Fedha za mfuko wa Jimbo ni za Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri na yeye anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni miradi ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa imekwishaidhinishwa na vikao husika,” aliongeza.

Alisema makusanyo ya fedha yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha hizo zinavyotumiwa. 

“Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila diwani. Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo,” alisisitiza.

Alisema kuna baadhi ya watu wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia kutumia fedha hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building).

“Hii si sahihi na jana nimepiga marufuku posho za aina hii pamoja na fedha za vitafunwa kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na waliozikusanya hawapati chochote,” aliongeza.

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu aliwataka waangalie baadhi ya makampuni ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini wanatumia software ambazo zinawanufaisha na wao pia.

“Tumieni watu wenu wa TEHAMA kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile mashine siyo waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna mianya ya wizi. Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia kwenye akaunti za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu wanayoijua wao. Ukiangalia unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia unaibiwa. Jaribuni kuchunguza na mjiridhishe na hizo software zao,” alisisitiza.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
habari mpekuzihuru

Zaidi Ya Bilioni 4 Zakusanywa Na Kikosi Cha Usalama Barabarani Mkoa Wa Arusha Kutokana Na Makosa Ya Barabarani

Jumla ya shilingi  4,708,680,000 zimekusanywa na jeshi la polisi mkoa wa Arusha kikosi cha usalama barabarani kutokana na faini zilizolipwa na watumiaji wa vyombo vya  moto  kwa kipindi cha January 2016 hadi December 2016 hiii ikiwa ni ongezeko kubwa tofauti na miaka iliopita

Hayo yamebainishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles   Mkumbo wakati akiongea na waandishi wa habari  kwa ajili ya kutoa taarifa ya hali ya usalama kwa kipindi chote cha mwaka 2016 kuanzia Januari hadi Disemba  ambapo alisema kuwa kwa upande wa ukusanyaji wa notification  fedha zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa  tozo hizo za notificationi katika kipindi cha mwaka 2016 ziliongezeka hadi kufikia shilingi 4,708,680,000/=  tofauti na mwaka 2015 ambapo jumla ya shilingi 3,227,640,00/= zilikusanywa kwa  hivyo kutokana na takwimu hizo kikosi cha usalama barabarani kimekusanya ongezeko la zaidi ya shilingi 1,481,040,000/=.

“Fedha hizi zimeongezeka kutokana na makosa mbalimbali yanayofanywa na madereva mbalimbali wa vyombo vya moto kwa kujua wanavunja sheria ,na wengine wakiwa wanafanya kwa kutokujua sasa sisi kama jeshi la polisi tunatumia njia ya kuwaonya kwa kuwatoza faini ili waweze kujirekebisha  kwa haraka kwa sababu tusipo fanya hivyo na kuwaonya bila kuwapiga faini watakuwa wanarudia makosa kila siku ,na pia ongezeko hilo limetokana na kuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaotumia vyombo vya moto ,mfano ukiangalia  magari mjini uwezi kufananisha magari yaliyokuwepo mwaka jana na mwaka huu mwaka huu yameongezeka kwa kasi na hata pikipiki pia ni hivyo hivyo”alisema Mkumbo.habari na mpekuzihuru

Amuua mkewe kwa nyundo Kisa Wivu wa Mapenzi

Mwanamke mmoja mkazi wa Mikumi wilayani Keya, Mbeya aliyefahamika kwa jina la HILDA SIGARA  amefariki dunia akiwa anapelekwa Hospitali kwa matibabu baada ya kupigwa nyundo kichwani na mume wake aitwaye REBSON TWEVE umri kati ya miaka 30 – 35

Kamanda wa polisi mkoani humo DCP Dhahiri Kidavashari amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 05.01.2017 majira ya saa 12:00 asubuhi ambapo imedaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani inasadikiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.

Amesema katika eneo la tukio kumekutwa nyundo moja, kisu kimoja na fimbo ya muanzi ambavyo vinasadikiwa kutumika katika tukio hilo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Kyela ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na upelelezi unaendelea huku mtuhumiwa akiwa ametoroka mara baada ya tukio na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Aidha, katika matukio mengine kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi limepokea taarifa za kujinyonga kwa watu wawili ambao miili yao imekutwa ndani ya nyumba zao katika maeneo tofauti.

Watu hao ni pamoja EDWARD PETER  mfanyabiashara na Mkazi wa Majengo na aliyekutwa amekufa chumbani kwake huku mwili wake ukiwa hauna majeraha yoyote, na mwingine ni ROBERT MWAISENYE Mkazi wa Mbugani wilayani Chunya ambaye alikuwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila akiwa ndani ya nyumba yake.habari na mpekuzihuru