Thursday 5 January 2017

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humprey Polepole atangaza neema kwa Wanafunzi waliokosa mikopo

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM, Humprey Polepole amewatangazia neema wanafunzi wa elimu ya juu waliokosa mikopo, akiwataka wamtafute ili awaoneshe cha kufanya

Polepole ambaye alikuwa kwenye kipindi cha Kikaangoni cha EATV aliuzwa na baadhi ya watu kuhusu tatizo lililopo la mikopo ya elimu ya juu, ambapo aliwajibu kuwa serikali imekwishatoa maelekezo kwamba haiwezi kumkopesha kila mtu na kwamba inatoa mikopo kwa vigezo vilivyowekwa.

Kuhusu watu wasioweza kujigharamia elimu hiyo na wamekosa mikopo, amewashauri kuahirisha masomo yao, ili wafanye kazi ambazo zitawasaidia kupata pesa na ndani ya mwaka mmoja ana uhakika watakuwa wamepata pesa zinazohitajika na kuendelea na masomo yao.

Polepole alitaja baadhi ya shughuli ambazo angewashauri wazifanye kuwa ni pamoja na kilimo huku akitolea mfano baadhi ya watu aliowashauri wajiingize kwenye kilimo cha matikiti na wakaufanyia kazi ushauri huo, ambapo baada ya muda wameona matunda yake.

"Waliokosa mikopo vyuo vikuu wanitafute, nitawaonesha cha kufanya, na wawe tayari kuahirisha masomo mwaka mmoja"

Akizungumzia uamuzi wa serikali kusimamisha ajira, Polepole amesema serikali haiwezi kuendelea kuajiri wakati inafanya kazi ya kuondoa wafanyakazi hewa ambao wanalitia hasara taifa na kuwataka watanzania waendelee kuwa watulivu na kumuunga mkono Rais Magufuli, ili amalize mchwa wote serikali na kisha ajira zitatoka.

"Nawaambia vijana wakati unasubiri ajira usibweteke kwani mtu anayebweteka akipata kazi ataharibu kazi yetu"

Kuhusu serikali kuajiri walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati pekee, Polepole amesema uamuzi huo ni sahihi kwa kuwa taifa lina uhaba mkubwa wa walimu wa Sayansi na Hisabati kuliko walimu wa masomo ya sanaa.

"Tunao utimilifu wa walimu wa sanaa, tunao upungufu wa walimu wa Sayansi"
habari mpekuzihuru

Kafulila kupokea kadi ya Chadema jimboni Kwake Mwezi Huu

Aliyekuwa  Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amesema atapokelea kadi ya Chadema jimboni mwake baadaye mwezi huu.

Kafulila alitangaza kuhama NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema kwa alichoeleza kuwa ndicho chama kilichojipambanua kuelekea safari ya mabadiliko ifikapo mwaka 2020.

Kada huyo tayari amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kuwa anajivua uanachama na  anarudi Chadema.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Kafulila alisema ameamua kuwa atapokelea kadi hiyo jimboni kutokana na mapenzi aliyonayo kwa wananchi wake.

"Nimepanga kuchukua kadi mwezi huu jimboni, kwa kuwa ilikuwa nichukue kadi mwanzoni lakini ilishindikana kutokana na siku kuu, hivyo siku yoyote kuanzia sasa nitachukua," alisema.

Wakati anajiuzulu NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema, alisema hakufanya uamuzi kwa kukurupuka bali alitafakari na kushauriwa na wananchi wa jimbo lake, na kuridhika kurudi huko.

"Nilitafakari na kushauriwa sana jimboni na kuridhika kwamba Chadema ndiko sehemu inayojipambanua kwa mikakati ya kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania na ni vema kukusanya nguvu ya kila mwenye kiu ya mabadiliko ndani ya chama kimoja, ili kufupisha safari ya mabadiliko," alisema.

Alipoulizwa kwa nini amerudi Chadema wakati aliyekuwa Katibu  Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa alipata kumwita sisimizi kwa  alichoeleza kuwa hakuwa na imani naye, alijibu kuwa siasa ni malengo si uhusiano binafsi.

Kafulila aliongeza kuwa wanasiasa wanaunganishwa na malengo zaidi ya urafiki na kwamba malengo yake sasa ni kuendelea kupigania mabadiliko ya kimfumo yanayoenea zaidi kwenye chama hicho (Chadema) kuliko kingine.

Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua uanachama wa Chadema na kuhamia NCCR-Mageuzi kutokana na kuondolewa kwenye nafasi ya uofisa habari wa chama hicho.

Pia akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa uanachama kwa kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka 'kumpindua' Mwenyekiti, James Mbatia.

Hata hivyo, suala hilo lilipata suluhu baada ya Mbatia kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Mbunge. Wakiwa bungeni, Mbatia na Kafulila walikutana, kuzungumza na hatimaye kumaliza mzozo wao.
habari mpekuzihuru

Waziri Mkuu aagiza akiba ya mahindi itunzwe hadi msimu ujao wa Mavuno........ RC, Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.

“Angalieni ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”

“Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,”alisisitiza.

“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,”alisisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.

Alisema kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.

“Kanda ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.

“Kanda ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu utakapokamilika.”

Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.

Alipolizwa ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila mwaka).

“Kuimarika kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. 

“Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.

Waziri Mkuu leo anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
habari mpekuzihuru

Waziri Mkuu apiga marufuku Madiwani kupewa fedha za maendeleo mikononi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini kuacha kutoa fedha taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.

Badala yake amewataka waandae mfumo maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za mfuko wa Jimbo ambazo ni maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za maendeleo jimboni.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo Manispaa ya Songea.

“Nimepata taarifa kuwa fedha za maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana. Msiwape fedha mkononi, bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na matumizi ya aina hiyo, mwisho wake ni jana,” alisisitiza.

“Fedha za mfuko wa Jimbo ni za Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri na yeye anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni miradi ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa imekwishaidhinishwa na vikao husika,” aliongeza.

Alisema makusanyo ya fedha yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha hizo zinavyotumiwa. 

“Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila diwani. Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo,” alisisitiza.

Alisema kuna baadhi ya watu wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia kutumia fedha hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building).

“Hii si sahihi na jana nimepiga marufuku posho za aina hii pamoja na fedha za vitafunwa kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na waliozikusanya hawapati chochote,” aliongeza.

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu aliwataka waangalie baadhi ya makampuni ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini wanatumia software ambazo zinawanufaisha na wao pia.

“Tumieni watu wenu wa TEHAMA kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile mashine siyo waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna mianya ya wizi. Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia kwenye akaunti za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu wanayoijua wao. Ukiangalia unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia unaibiwa. Jaribuni kuchunguza na mjiridhishe na hizo software zao,” alisisitiza.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
habari mpekuzihuru

Zaidi Ya Bilioni 4 Zakusanywa Na Kikosi Cha Usalama Barabarani Mkoa Wa Arusha Kutokana Na Makosa Ya Barabarani

Jumla ya shilingi  4,708,680,000 zimekusanywa na jeshi la polisi mkoa wa Arusha kikosi cha usalama barabarani kutokana na faini zilizolipwa na watumiaji wa vyombo vya  moto  kwa kipindi cha January 2016 hadi December 2016 hiii ikiwa ni ongezeko kubwa tofauti na miaka iliopita

Hayo yamebainishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles   Mkumbo wakati akiongea na waandishi wa habari  kwa ajili ya kutoa taarifa ya hali ya usalama kwa kipindi chote cha mwaka 2016 kuanzia Januari hadi Disemba  ambapo alisema kuwa kwa upande wa ukusanyaji wa notification  fedha zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa  tozo hizo za notificationi katika kipindi cha mwaka 2016 ziliongezeka hadi kufikia shilingi 4,708,680,000/=  tofauti na mwaka 2015 ambapo jumla ya shilingi 3,227,640,00/= zilikusanywa kwa  hivyo kutokana na takwimu hizo kikosi cha usalama barabarani kimekusanya ongezeko la zaidi ya shilingi 1,481,040,000/=.

“Fedha hizi zimeongezeka kutokana na makosa mbalimbali yanayofanywa na madereva mbalimbali wa vyombo vya moto kwa kujua wanavunja sheria ,na wengine wakiwa wanafanya kwa kutokujua sasa sisi kama jeshi la polisi tunatumia njia ya kuwaonya kwa kuwatoza faini ili waweze kujirekebisha  kwa haraka kwa sababu tusipo fanya hivyo na kuwaonya bila kuwapiga faini watakuwa wanarudia makosa kila siku ,na pia ongezeko hilo limetokana na kuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaotumia vyombo vya moto ,mfano ukiangalia  magari mjini uwezi kufananisha magari yaliyokuwepo mwaka jana na mwaka huu mwaka huu yameongezeka kwa kasi na hata pikipiki pia ni hivyo hivyo”alisema Mkumbo.habari na mpekuzihuru

Amuua mkewe kwa nyundo Kisa Wivu wa Mapenzi

Mwanamke mmoja mkazi wa Mikumi wilayani Keya, Mbeya aliyefahamika kwa jina la HILDA SIGARA  amefariki dunia akiwa anapelekwa Hospitali kwa matibabu baada ya kupigwa nyundo kichwani na mume wake aitwaye REBSON TWEVE umri kati ya miaka 30 – 35

Kamanda wa polisi mkoani humo DCP Dhahiri Kidavashari amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 05.01.2017 majira ya saa 12:00 asubuhi ambapo imedaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani inasadikiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.

Amesema katika eneo la tukio kumekutwa nyundo moja, kisu kimoja na fimbo ya muanzi ambavyo vinasadikiwa kutumika katika tukio hilo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Kyela ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na upelelezi unaendelea huku mtuhumiwa akiwa ametoroka mara baada ya tukio na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Aidha, katika matukio mengine kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi limepokea taarifa za kujinyonga kwa watu wawili ambao miili yao imekutwa ndani ya nyumba zao katika maeneo tofauti.

Watu hao ni pamoja EDWARD PETER  mfanyabiashara na Mkazi wa Majengo na aliyekutwa amekufa chumbani kwake huku mwili wake ukiwa hauna majeraha yoyote, na mwingine ni ROBERT MWAISENYE Mkazi wa Mbugani wilayani Chunya ambaye alikuwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila akiwa ndani ya nyumba yake.habari na mpekuzihuru

Tuesday 3 January 2017

Mbunge Lwakatare wa CHADEMA Ammwagia Sifa Rais Magufuli

Serikali Yafuta Posho Za Vitafunwa, Mazingira Magumu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Ametia agizo hilo leo (Jumanne, Januari 3, 20017) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Kuanzia sasa marufuku Wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.

Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na Halmashauri na Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa kwenye miradi na shughuli za maendeleo.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Katika halmashauri zetu kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato hadi walinzi, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya leo atakuwa amejifukuzisha kazi.

Aidha, ameagiza fedha zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala yake zipelekwe kwenye kata husika na zifuatiliwe matumizi yake.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa kwenye halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Pia amewataka watumishi wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri hiyo ambao wamehamishiwa kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika Manispaa hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu yao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
habari na mpekuzihuru

EWURA yatangaza bei mpya za mafuta

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA)  imetangaza bei mpya za nishati ya mafuta zitakazoanza kutumika kesho Jumatano huku bei ya mafuta ya taa na dizeli ikiwa imeshuka kwa wastani wa shilingi 66 kwa lita.

Taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Felix Ngamlagosi inaonesha kuwa kwa wastani kumekuwa na ongezeko dogo sana la bei ya mafuta ya petroli ambayo kwa jiji la Dar es Salaam bado itauzwa kwa bei ile ile ilivyokuwa mwezi uliopita.

Hata hivyo, taarifa hiyo imetoa ruhusa kwa wauzaji wa jumla na rejareja wa mafuta nchini kuuza bidhaa hiyo kwa bei ndogo chini ya bei elekezi iliyotangazwa na mamlaka hiyo kama njia ya kuchochea ushindani baina ya wauzaji wa mafuta nchini.
habari na mpekuzihuru

Utata Wagubika Mauaji ya Afisa Mtendaji Mbeya

Mwili wa ofisa mtendaji wa mtaa wa Kabwe, katika kata ya Iyela jijini Mbeya Clementine Enock (34) umekutwa ukiwa umetelekezwa katika eneo la Airport ya zamani baada ya kuuawa na watu wasiofahamika kwa kubanwa pumzi.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa walibaini kuwepo kwa mwili huo Januari mbili, mwaka huu majira ya saa moja asubuhi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Kidavashari alifafanua kuwa kabla ya tukio hilo marehemu aliondoka nyumbani kwao siku ya Mwaka mpya  na kuaga kuwa anakwenda Airport kwenye sherehe ya rafiki yake huku akiwa na gari yenye namba za usajili T234 DJM aina ya Toyota Spacio.

Alisema kuwa ndugu wa marehemu walipata hofu mara baada ya ndugu yao kuchelewa kurudi nyumbani na ndipo wakaanza kumpigia simu bila mafanikio mpaka usiku wa manane.

“Marehemu aliaga nyumbani kwao Uyole ya Kati alikokuwa akiishi majira ya saa kumi jioni siku ya tarehe moja kwa madai anaenda kwenye sherehe ya rafiki yake akiwa na usafiri wa gari lake, ambapo mpaka kufika usiku wa manane hakukuwa na taarifa yeyote ndipo hofu ikatanda kwa familia ambapo walipiga simu kwa ndugu jamaa na marafiki na kueleza kuwa hawajui alipo,” alisema Kidavashari.

Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari siku iliyofuata majira ya saa moja asubuhi mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umetupwa katika eneo la wazi jirani na Shule ya Sekondari ya Samora ambapo uchunguzi wa awali unaonesha kifo chake kilitokana na kubanwa pumzi na watu wasiofahamika.

Alisema mazingira ya kifo yanaonyesha wazi kuwa marehemu aliuawa na mtu wa karibu yake huku akisema tukio hilo lilifanywa ndani ya nyumba ya mtu.
habari na mpekuzihuru

TCRA Yatishia Kuzifutia Leseni Kampuni za Simu

Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imetishia kusitisha kwa muda au kufuta kabisa leseni ya biashara kwa kampuni zote za mawasiliano nchini, zitakazoshindwa kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)

Hatua hiyo ni kulingana na sheria mpya ya fedha ambayo imetoa ukomo wa hadi Desemba 31 mwaka jana kampuni hizo ziwe zimejisajili katika soko hilo.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hii leo; Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba amesema kwa sasa wanasubiri maelezo kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana  (CMSA) kuhusu idadi ya kampuni za mawasiliano zilizokidhi sifa za kusajiliwa katika soko la hisa kwa ajili ya kuchukua hatua kwa zile zilizokaidi kutekeleza agizo hilo la kisheria.

Mhandisi Kilaba amesema TCRA imeikabidhi CMSA orodha ya kampuni zaidi ya 80 za mawasiliano, orodha ambayo CMSA itaipitia kwa lengo la kuchuja na kupata kampuni ambazo zinastahili kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Kauli ya Mhandisi Kilaba imekuja huku taarifa kutoka soko la Hisa la Dar es Salaam zikionesha kuwa ni kampuni tatu pekee ndizo zimejisajili katika soko hilo, licha ya muda wa kufanya hivyo kufikia ukomo wake Jumamosi ya Desemba 31 mwaka jana.habari na mpekuzihuru

Serikali kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.........Wale wa Maomo Mengine Watulie Maana Hakuna Uhaba Kwa Sasa

Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa katika ziara yake ya kutembela wilaya mpya za jiji hilo, akianzia na Kigamboni siku ya leo.

Majaliwa amesema mchakato wa ajira hizo unaendelea chini ya Ofisi ya Rais Utumishi, na muda wowote kutoka sasa mchakato huo utakapokamilika, majina yatatolewa na walimu hao kuajiriwa.

Kuhusu walimu wa masomo mengine, Waziri Mkuu amesema walimu wa masomo mengine hususani ya sanaa wapo wa kutosha na kwamba wanapaswa kusubiri kwakuwa wao wako wengi zaidi na hakuna uhaba na uhitaji wa walimu hao wa masomo ya sanaa.

Hivi karibuni, Wizara ya Elimu iliwataka wahitimu wa ualimu katika masomo ya sayansi na hisabati kutuma taarifa (CV) zao ili izihakiki kabla ya ajira, mchakato ambao tayari umekamilika na majina yalitumwa katika wizara ya utumishi.

Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya wiki mbili zilizopita wakati akiongea na kituo cha EATV alisema kuwa kazi ya wizara yake ilikuwa ni kuhakiki taarifa za wahitimu hao, na si kuajiri, huku akibainisha kuwa zoezi hilo limekamilika na majina yako utumishi ambao ndiyo watahusika na kuajiri.

Pia alisisitiza kuwa kama wizara ya elimu waliomba kupewa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati haraka kwa kuwa uhitaji wao ni mkubwa zaidi na kuwataka wahitimu wote waliotuma taarifa zao, wasubiri watapata majibu muda si mrefu.
habari na mpekuzihuru

Polisi kufukua kaburi la binti aliyezikwa kwa siri Arusha

Familia moja  jijini Arusha inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa kike wa miaka mitatu katika kaburi lililofichwa, huku majirani wakidanganywa kuwa binti huyo yupo hai.

Taarifa za kisa hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama. Kwa sasa kuna mipango ya kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru Losipha aliyezikwa kwa siri na familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi zaidi.

Inadaiwa kuwa Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au ukeketaji na ngariba, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku familia yake ikishuhudia.

Kitendo hicho kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti wilayani Arumeru Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku tatu tu, kabla ya mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, hajaingia mwaka mpya wa 2017.

Mtendaji wa Kata ya Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na taarifa hizo hadi vyombo vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa uchunguzi na ndipo alipolazimika kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi cha Ngaramtoni.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na liwe na kwamba ikiwezekana kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo asiye na hatia, uchunguzwe upya.

“Ndio kwanza nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha mahakama ili twende kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli mtoto huyo amezikwa humo na iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza uchunguzi juu ya kifo chake,” alisema Kamanda arles Mkumbo.

Baba wa marehemu, Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki kutokana na ugonjwa wa baridi yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi kirefu kabla ya kupoteza maisha Desemba 28, mwaka jana. Lakini madai yake hayo yanapingana na ripoti ya muuguzi katika duka la dawa lililopo kijiji cha jirani cha Kidali, anayeitwa Jane Andrew.

“Walimleta mtoto hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia na kutokwa na damu nyingi,” alidai.

Muuguzi huyo aliwahimiza wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea hadi ripoti za kifo zilipomfikia.

Huku serikali ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado kuna familia nyingi kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa, zinaendeleza mila hiyo kwa siri.

Kwa sasa familia hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa wadogo sana, kuepuka kukamatwa.

Ngariba wanaotumika kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe wasiokuwa na ujuzi, taaluma za afya na hutumia vifaa butu, ambazo husababisha uvujaji mwingi wa damu na kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa mengine.
habari na mpekuzihuru

Mlinzi mwingine auawa Geita....Aliyepigwa na wafugaji Morogoro Afariki Dunia

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi
 Mauaji ya walinzi mkoani Geita yamendelea kuwa tishio kwa usalama wao baada ya mlinzi mwingine aliyekuwa akilinda maduka yapatayo 15, kuuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani. 

Mauaji ya mlinzi huyo Kisusi Iddy (40) aliyekuwa akilinda maduka hayo kwenye Mtaa wa Mwatulole, ni muendelezo wa matukio ya kuuawa walinzi wa maduka na mali mbalimbali kwani katika kipindi cha miaka miwili  jumla ya walinzi 20 wameuawa. 

Taarifa zilizopatikana jana kuhusu mauaji ya mlinzi huyo na kuthibitishwa na mwenyekiti wa mtaa huo, Fikiri Toi zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari Mosi na wauaji hao hawakuiba kitu chochote. 

Mwili wa Iddy ulikutwa umefunikwa kwa shuka lake alilokuwa akilitumia lindoni, huku likiwa limetapakaa damu. 

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amefuta vibali vyote vya waganga wa tiba za asili kwa madai wao ni moja ya chanzo cha imani za kishirikina zinazosababisha mauaji hayo.

 Alisema kutokana na kukithiri kwa mauaji hayo, mamlaka yake inakusudia kufufua Jeshi la Jadi (Sungusungu) ili kusaidia kuyadhibiti. 

Hata hivyo, Kapufi alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa wakati wa uhai wake, Iddy alikuwa analinda maduka ya wafanyabiashara yanayofikia 15 na kwamba baada ya kufuatilia, hakuwa na mafunzo yoyote ya ulinzi.

 Aliyepigwa na wafugaji Moro afariki 
Fabian Bago (21) anayedaiwa kushambuliwa na wafugaji katika Kijiji cha Kolelo, Morogoro, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Frank Jacob alisema kijana huyo alifariki dunia saa 11 jioni jana akiwa kwenye wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu na kwamba mwili wake umehifadhiwa kusubiri taratibu nyingine za kipolisi.

 Dk Jacob alisema mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, kijana huyo alifanyiwa vipimo na matibabu lakini alifariki dunia kutokana na majeraha makubwa kichwani yaliyoharibu sehemu ya ubongo. 

Baba mzazi wa kijana huyo, Alan Bago alisema ameshatoa taarifa polisi kuhusina na kifo cha kijana wake na sasa anasubiri maelekezo ya polisi ili aweze kuendelea na taratibu za mazishi.habari na mpekuzihuru

Zitto Kabwe Adai Kuna Uhaba Mkubwa wa Chakula Nchini.........Waziri wa Kilimo Ampinga

Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akidai kuwa hali ya chakula nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya, Serikali imesema hali ni shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za wastani. 

Zitto alidai jana kuwa Ghala la Taifa la Chakula (SGR) lina hifadhi ya chakula kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015 kulikuwa na chakula cha kutosha miezi miwili. 

Kwa mujibu wa Zitto, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Novemba inaonyesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), imebaki na tani 90,476 tu za chakula ambacho amedai ni cha kutosholeza siku nane.

 Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alijibu madai hayo ya Zitto akisema nchi ina chakula cha kutosha wala siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi. 

Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi. 

“NFRA inanunua chakula kwa kuangalia mahitaji kwa mwaka huo ukoje, watu wakivuna sana maghala yao yanakuwa yamejaa na mahitaji ya chakula yanakuwa madogo ndiyo maana Serikali hainunui chakula kingi. Miaka miwili iliyopita Serikali ilinunua mahindi kwa wingi lakini yaliishia kuharibika,” alisema Dk Tizeba. 

Aliongeza kuwa Serikali sasa ina mradi wa kujenga ghala jingine lenye uwezo wa kuhifadhi tani 260,000 ili likiungana na la sasa lenye uwezo wa tani 246,000 nchi iwe na uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya 500,000. 

“Kuna maeneo mahindi yameanza kukomaa na wakulima wa huko watavuna kama kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa chakula nje ya nchi bila vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo siwezi kutaja kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila kinatosha siyo kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,” alisema Tizeba. 

Juzi wakati akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani katika kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Zitto alisema kauli ya Rais John Magufuli kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera kwamba Serikali haina shamba ni kuficha uamuzi unaosababisha kukosekana kwa akiba ya chakula ya kutosha. 

Alidai kuwa hali ya chakula nchini si nzuri, wananchi wanashuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku akidai kuwa bei ya sembe na mchele zimekuwa juu na gharama za maisha zitaendelea kupanda kutokana na uhaba wa chakula kuwa mkubwa.

 “Hali ya chakula inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya Serikali kuhusu hifadhi ya chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa chakula hicho kiingie sokoni, hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula,” alisema Zitto. 

Aliongeza kuwa mpaka sasa NFRA ina tani 90,476 za chakula wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 ghala la chakula lilikuwa na tani 459,561. 

Takwimu alizozitoa Zitto Kabwe alizinukuu katika ripoti ya BoT ya Novemba mwaka jana ambayo inaonyesha kuwa tangu Januari 2016 hadi Julai 2016, akiba ya chakula ilipungua kutoka tani 125,668 hadi 49,632, lakini hadi Oktoba mwaka huo iliongezeka hadi 90,476. 

Ripoti hiyo inaonyesha tofauti ya uhifadhi wa chakula kwa mwaka jana na miaka mingine miwili iliyotangulia kwani mwaka 2014 Januari, kulikuwa na tani 235,309 na Desemba, tani 466,583 huku mwaka mwaka 2015 Januari kukiwa na tani 459,561 na Desemba 180,746. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Steven Ruvuga alisema hali halisi kwa wakulima siyo nzuri kwa kuwa mvua zilinyesha chini ya kiwango, hivyo kuna hofu ya ukosefu wa chakula cha kutosha baadaye. 

“Sasa hivi nipo Kiteto na kwa kawaida mahindi yalipaswa kuwa tayari yameinuka kufikia walau mabega ya mtu mzima, lakini nikiyatizama sasa bado yako chini. 

"Mwaka huu kuna hatari ya ukosefu wa chakula na naishukuru Serikali kwa kuwa imeanza kuchukua hatua katika maeneo yenye uhitaji,”alisema Ruvuga. 

Aliongeza kuwa Ghala la Taifa linapaswa kuwa na wastani wa tani 300,000 za akiba lakini kama sasa zipo 90,476 zinaweza zisikidhi mahitaji ya kila mtu hivyo ni vyema ikabuni mpango mbadala.habari na mpekuzihuru