Tuesday 3 January 2017

Serikali kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.........Wale wa Maomo Mengine Watulie Maana Hakuna Uhaba Kwa Sasa

Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa katika ziara yake ya kutembela wilaya mpya za jiji hilo, akianzia na Kigamboni siku ya leo.

Majaliwa amesema mchakato wa ajira hizo unaendelea chini ya Ofisi ya Rais Utumishi, na muda wowote kutoka sasa mchakato huo utakapokamilika, majina yatatolewa na walimu hao kuajiriwa.

Kuhusu walimu wa masomo mengine, Waziri Mkuu amesema walimu wa masomo mengine hususani ya sanaa wapo wa kutosha na kwamba wanapaswa kusubiri kwakuwa wao wako wengi zaidi na hakuna uhaba na uhitaji wa walimu hao wa masomo ya sanaa.

Hivi karibuni, Wizara ya Elimu iliwataka wahitimu wa ualimu katika masomo ya sayansi na hisabati kutuma taarifa (CV) zao ili izihakiki kabla ya ajira, mchakato ambao tayari umekamilika na majina yalitumwa katika wizara ya utumishi.

Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya wiki mbili zilizopita wakati akiongea na kituo cha EATV alisema kuwa kazi ya wizara yake ilikuwa ni kuhakiki taarifa za wahitimu hao, na si kuajiri, huku akibainisha kuwa zoezi hilo limekamilika na majina yako utumishi ambao ndiyo watahusika na kuajiri.

Pia alisisitiza kuwa kama wizara ya elimu waliomba kupewa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati haraka kwa kuwa uhitaji wao ni mkubwa zaidi na kuwataka wahitimu wote waliotuma taarifa zao, wasubiri watapata majibu muda si mrefu.
habari na mpekuzihuru

No comments:

Post a Comment